Choose the correct answer for each question.
Nchi za Afrika ya Mashariki zimebarikiwa na kila aina za sanaa za maumbile. Tukienda sehemu ya pwani tunaweza kuona ufuko mzuri na safi sana. Tukienda bara tunaweza kuona milima na maumbile ya kupendeza machoni. Kwa hivyo, kama mnavyojua bila shaka, nchi za Kenya na Tanzania zinatembelewa na wageni wengi kutoka nchi mbalimbali haswa nchi za Ulaya na Amerika.
Wageni hawa, yaani watalii, ni muhimu kwa uchumi kwa nchi hizo kwa sababu wanaleta fedha za nje za kigeni. Basi, wageni hupokewa kwa ukarimu mwingi wakifika Kenya na Tanzania. Kuna mahoteli na misafara ya kila aina kote nchini ili wageni wasipate taabu yo yote.
Kama tunavyojua, Kenya na Tanzania zina wanyama wa mwitu wa aina nyingi kama simba, chui, tembo, na punda milia na wengine wengi. Ni wanyama hao wanaovutia wageni wengi. Ni ajabu kwa wageni kuona wanyama wakitembea huru katika maskani yao kama huko Serengeti1 ambako wanyama ni wengi mno, hasa maelfu ya nyumbu, punda milia, na swala. Ni ajabu kuona nyumbu hao wote ambao ni wengi kuliko wanyama wote wengine kule.
Wageni pia hupenda kutembelea watu wa sehemu mbalimbali za nchi hizi mbili na kuona wanavyoishi na mila na desturi zao. Wengine pia hupenda kuona na kujaribu kupanda Mlima wa Kenya na Mlima wa Kilimanjaro. Kilimanjaro ni mlima mrefu zaidi kuliko yote bara ya Afrika. Wengine hupenda kutembelea miji ya pwani, haswa miji ya zamani kama Malindi na Lamu, ambayo ni miji ya pwani ya Kenya. Kwa hakika, ukitembelea Kenya au Tanzania utajua kwa nini wageni wanazipenda mno nchi hizo.